Skip to main content

Aina bora za ng’ombe wa maziwa, banda na namna ya kuanza ufugaji


Image result for PERSIAN COW IMAGE

Uzalishaji wa maziwa ni biashara nzuri sana na ya kuvutia ambayo huwa na faida nyingi na humfanya mfugaji kuridhika hasa kwa yule anayependa kazi hii. Hata hivyo, ni lazima kuanza kwa kuweka msingi imara hata kabla ya kufikiria ni aina gani ya mbegu utaichukua kwa ajili ya kufuga. Ni vizuri kufahamu kuwa, usimamizi ni moja ya jambo muhimu sana ambalo likifanyiwa uzembe linaweza hata kumbadilisha ng’ombe wa maziwa kuwa na uzalishaji duni kama ngo’mbe wa kienyeji.

Aina mbalimbali za ng’ombe wa maziwa huwa na mahitaji tofauti, hivyo kiwango cha maandalizi yako ni muhimu sana. Unahitajika kufahamu kuwa, unalazimika kufikia mahitaji yako kwa ajili ya lishe, si kwenye mahitaji ya awali tu bali pamoja na mahitaji ya baadaye ya ngo’mbe wako. Suala hili limefanya wafugaji wengi kushindwa kuendelea kutokana na kuwa hujiingiza katika shughuli hii bila kuangalia mambo ya msingi yanayotakiwa pamoja na kuweka mipango thabiti.

Pamoja na kuwa mahitaji yote kwa ajili ya lishe na mambo mengine yako sawa, ng’ombe wa maziwa ni lazima kuzalisha kulingana na umbile lake na uwezo wake kamili. Kama utaweza kumudu kufuga ng’ombe halisi wa maziwa, ni lazima pia utambue kuwa uzalishaji wa juu wa maziwa uhitaji pia usimamizi wa hali ya juu. Kwa maana hiyo, ni vyema kufuga ng’ombe wa kiwango cha kawaida (ikiwezekana chotara) ambaye ataendana na uwezo wako wa kumtunza.

Ni vyema tukaangalia aina mbili za ng’ombe wa maziwa ambao wana uwezo wa kuzalisha maziwa mengi;

(i) Freshiani (Friesian)
Ng’ombe aina ya freshiani ni rahisi kumtambua kutokana na kuwa na rangi nyeusi na nyeupe, na ni ng’ombe wenye uzalishaji bora wa maziwa. Wanyama hawa ni wakubwa na pia wanaweza kuwa na mabaka meupe na meusi au mekundu na meupe. Ikiwa watalishwa vizuri, freshian aliyefikia umri wa kukomaa huwa na uzito wa hadi kilogramu 550 na urefu wa sentimeta 150 kutoka begani. Mtamba huweza kupandwa, akiwa na umri wa miezi mitano huku akiwa na uzito wa kilogramu 360.

Wakati baadhi ya ng’ombe wakiwa na uwezo wa kuishi kwa muda mrefu, uwezo wa kawaida wa kuishi kwa Freshiani ni miaka sita. Hata hivyo, aina hii ya ng’ombe ni wazalishaji wazuri wa maziwa ambao huweza kuzalisha kilogramu 7800 kwa wastani kwa muda wa siku 360 yakiwa na kiwango cha chini cha mafuta ikilinganishwa na aina nyingine ya ng’ombe.

Aidha, aina hii ya ng’ombe huhitaji ulishaji mkubwa hivyo hushauriwa kwa wafugaji wenye uhakika wa kuwa na lishe bora na ya kutosha kwa mwaka mzima.

(ii) Ayrshire
Aina hii ng’ombe huwa na miraba ya kahawia na nyeupe karibu sawa na aina nyingine ya ng’ombe ambao huelekea kuwa na rangi ya (Mahogany). Ng’ombe hawa huwa na wastani wa kawaida, na uzito wa kilogramu 540 katika umri wa ukomavu. Aidha, humudu aina yeyote ya ufugaji na si rahisi kupata matatizo yeyote ya miguu.

Ayrshire huweza kufanya vizuri katika malisho ya aina yeyote tofauti na aina nyingine ya ng’ombe wa maziwa. Kukiwa na usimamizi mzuri na ulishaji mzuri, wastani wa uzalishaji wa maziwa ni kilogramu 5400 ikiwa na kiwango cha juu cha mafuta ukilinganisha na Freshian. Aryshire ni aina nzuri kwa kufuga hasa kutokana na nguvu aliyonayo pamoja na uzalishaji mkubwa wa maziwa. Ng’ombe wa aina hii, hutambulika kwa kuwa na umbo zuri pamoja na chuchu zake kuonekana kuwa zenye ubora. Aidha, utungaji wa maziwa yake, umefanya maziwa yake kuonekana ni mazuri sana katika uzalishaji wa siagi na jibini.

Maziwa ya Ayrshire yanafahamika kama “maziwa bora ya kunywa” kutokana na uwezo wake wa kuwa na mafuta ya kutosha na kiasi kikubwa cha protini. Kwa mfugaji anayeanza, aina hii ya ng’ombe ni nzuri sana kuanza nayo kasha baadaye kuongeza freshiani baada ya uwezo wako wa kuhudumia kuwa imara. Mifugo ya asili ni ghali sana na ni ngumu pia kuwapata, hivyo basi, njia rahisi kwa wafugaji wa maziwa wanaoanza ni kutafuta ng’ombe bora wa kawaida ambao mara nyingi huwa ni chotara, kisha kuwaboresha kwa kutumia mbinu ya kupandikiza dume bora na mwenye uzalishaji mkubwa. Na hii huhitaji elimu ya kutosha kuhusu uchaguzi wa madume.

*Muhimu: Wakati wa kununua ng’ombe kwa ajili ya kufuga, ni vyema mfugaji ukatambua kuwa, wazalishaji wa maziwa mara nyingi hawauzi ng’ombe wao wenye uzalishaji mzuri, badala yake huuza wale ambao hawazalishi kwa kiwango kizuri, wale wenye matatizo kama kutokushika mimba, wenye matatizo ya joto na wale ambao hushambuliwa na magonjwa mara kwa mara. Kwa maana hiyo, pamoja na aina ya ng’ombe unayehitaji kununua, ni muhimu sana kuwa mwangalifu usije ukanunua ng’ombe mwenye shida yoyote kwani hapo ndipo mwanzo wa uzalishaji wako kuja kuwa wa matatizo na kutokufikia lengo.

Banda na nafasi kwa ajili ya ng’ombe wa maziwa

Kabla mfugaji hajafikiria kuhusu makazi ya ng’ombe wake, ni vyema sana kujiuliza ni kiasi gani cha mifugo utahitaji kuwa nao baada ya miaka kadhaa hivyo kukuwezesha kutenga nafasi ya kutosha kwa ajili ya mifugo utakayoleta.

Njia rahisi ya kulitambua hilo, ni kujiuliza ni kiasi gani cha mifugo ungependa kuwa nao baadaye na ni kiwango gani cha uzalishaji wa maziwa ungetarajia kufikisha kutoka kwa ng’ombe wako.

Swali la kwanza, ni muhimu sana kwa mfugaji kujiuliza, kwani kiwango cha mifugo hutokana na uwezo wa kiwango cha lishe utakachohitajika kulisha mara kwa mara. Kwa kawaida, ekari moja ya ardhi hutoshea kulisha ng’ombe wa maziwa aina ya Freshiani mmoja au Jesrey wawili tu.

Ng’ombe wa maziwa mmoja (Fresian, Guernsey, Jersey) kiasi cha tani 5 ya lishe ya majani mabichi au majani makavu kwa mwaka. Hii ni sawa na kilogramu 25,000 za matete au kiasi cha majani uliyoyaotesha kwenye ekari moja. Pamoja na usimamizi mzuri wa malisho ya nyasi, au mchanganyiko wa malisho kama mikunde au mimea kama desmodium, ni dhahiri kuwa bado utahitajika kuwa na angalau ekari ya ziada 0.75 ya eneo ili kuweza kulisha ng’ombe wako vizuri.

Kwa ujumla, ng’ombe wa maziwa huhitaji lishe kiwango kikubwa kuliko ng’ombe wa nyama, na mara nyingi huwa na uzalishaji mkubwa pale ambapo ubora wa lishe ni wa hali ya juu. Hali kadhalika, kama utazalisha malisho yako mwenyewe, bado utahitaji njia nyingine ya ziada ya kupata lishe ikiwa itatokea tatizo lolote katika malisho.

Jedwahi hili huonesha kiwango cha lishe kinachohitajika kwa aina mbalimbali ya ng’ombe wa maziwa, pamoja na ardhi kwa ajili ya kuzalishia malisho.

Ufugaji wa ndani
Katika ufugaji wa ndani, ng’ombe wanahitajika kuwekwa kwenye hali ya usafi, na makazi yao yawe na ulinzi wa kutosha na yenye kuwapatia uhuru. Wafugaji walio wengi wamekuwa wakiwekeza fedha nyingi katika kuwajengea mifugo, na mwishoni kuishia

kukosa fedha kwa ajili ya kulishia mifugo hiyo. Mfugaji anayeanza, anashauriwa kujengea mifugo yake makazi mazuri na ya gharama nafuu na baadaye kuendeleza mabanda hayo kutokana na mapato yanayopatikana.

Mambo ya kuzingatia katika ujenzi wa mabanda
Nafasi: Ng’ombe mkubwa anahitaji kuwa na nafasi ya kutosha kwa ajili ya chakula, kupumzika pamoja kufanya mazoezi jambo ambalo wafugaji walio wengi hawazingatii na badala yake huweka mifugo yao katika nafasi ndogo ambayo mwishoni hudidimiza ukuaji wa mnyama na uzalishaji kwa ujumla. Kwa mantiki hiyo, ng’ombe mmoja mkubwa anahitaji mita za mraba 8 mbali na eneo lake la kupumzikia. Njia rahisi ni kutenga eneo hili mbele ya zizi/banda. Kumbuka, unapokuwa na nafasi kubwa, ndipo unapotengeneza uzalishaji mzuri.

Paa: Ni vyema kukawa na paa kwa ajili ya kuilinda mifugo dhidi ya upepo, mvua pamoja na jua kali. Hakikisha paa linakuwa juu, ili kuipa uhuru mifugo yako kutembea ndani ya banda bila tatizo lolote. Hakikisha mteremko wa paa hauwezi kuathiri sehemu ya mifugo kupumzika na sehemu ya lishe hasa kwa kuruhusu maji kuingia katika sehemu hizo.

Sakafu: Hakikisha sakafu inakuwa na mfumo mzuri wa mifereji kwa ajili ya kuruhusu maji na mkojo kupita hivyo kuwaweka mifugo katika hali nzuri. Unaweza kutengeneza sakafu ya simenti ambayo ni rahisi kusafisha. Hata hivyo kwa kuwa inagharimu fedha, mfugaji anaeanza, anaweza kutumia udongo wa mfinyanzi au aina nyingine ya udongo mgumu kutengeneza sakafu. Endapo utasakafu banda, sakafu isiwe inayoteleza kwa kuwa ng’ombe wanaweza kuteleza na kuumia. Sakafu iwe na mwinuko kidogo na mwinuko uelekee sehemu ya kutiririshia mkojo na kutolea kinyesi.

Matandiko: Eneo ambalo mifugo hupumzikia, ni vyema kukawa na matandiko. Unaweza kutumia malighafi ya aina yeyote kavu ambayo huweza kunyonya mkojo na samadi. Matandiko hayo ni lazima kubadilishwa mara kwa mara.

Vihondi vya maji na chakula: Hakikisha kuna vihondi vya kutosha kwa ajili ya chakula na maji. Mabanda ni vyema yakawa karibu na vyanzo vya upatikanaji wa maji safi na salama. Kwa wastani, ng’ombe mmoja anahitaji kunywa maji kiasi cha lita kati ya 50 au 80 kwa siku sawa na ndoo 5 hadi 8 za maji (za ujazo wa lita 10).

Shimo la mbolea: Mifugo inayolishwa vizuri hutoa samadi nyingi hivyo huweza kuwa tatizo kwa watu wanaokuzunguka hasa ikiwa inatapakaa kila mahali na kusababisha kuwepo kwa harufu mbaya. Kama utafuga mifugo mingi katika eneo dogo bila kuwa na sehemu maalumu ya kuweka mbolea inayotokana na mifugo hiyo, basi ni dhahiri kuwa utasababisha kutokuelewana na majirani, lakini pia kutasababishia wanyama kukaa katika hali ya usumbufu. Ni vyema kuandaa shimo maalumu kwa ajili ya samadi hasa kwa ufugaji wa ndani, kabla ya kutumia kwa ajili ya kuweka kwenye mashamba ya malisho.

Namna ya kuanza ufugaji kwa urahisi
Kabla ya kuamua kufanya biashara ya uzalishaji wa maziwa, maandalizi mazuri ni moja ya sababu itakayokupa mwanga kufanikiwa au kutokufanikiwa. Hata kabla ya kuwaza nia aina gani ya ng’ombe utanunua, ni lazima kufikiri kwanza ng’ombe huyo utamlisha nini.

Fikiria lishe, fikiria nyasi
Ili kufuga ng’ombe, ni lazima uwe na lishe ya kutosha. Huwezi kumuendeleza ng’ombe kuzalisha wakati hauna lishe bora ya kutosha, ikiwa ni pamoja na nyasi, mikunde na majani ya nafaka. Moja ya njia nzuri ya kuzingatia ni nyasi. Mfugaji anayeanza, ni lazima kuzingatia haya kwa ajili ya lishe;



  • Hakikisha unatunza nyasi za asili zilizopo katika shamba lako la malisho
  • Ongeza kwa kuotesha majani mengine mapya katika shamba lako
  • Nunua malisho ambapo unaweza kuswaga mifugo yako kwenda kula
  • Kodisha au nunua eneo kwa ajili ya kuotesha malisho kisha kukata na kupeleka kulishia mifugo
  • Nunua majani kutoka kwa watu wanye malisho au wanaofanya bishara ya kuuza majani yaliyokatwa 

Comments

Popular posts from this blog

MAMBO KUMI YA KUFANYA KABLA YA MIAKA 25

1. Jifunze kuweka akiba ya fedha na iache bila kuigusagusa.   2. Tafuta mpenzi sahihi na tulia naye, panga maisha. 3. Ishi mahali pa peke yako, acha kuishi kwa wazazi au kupanga na nyumba na washkaji. 4. Lipa madeni yako ya zamani. Yote! 5. Tengeneza mwili ambao unataka halafu jitahidi kuu-maintain! Anza kuzingatia kuishi kwa kujali afya yako sana. 6. Jitahidi uwe na marafiki ambao wana changamoto za kimaendeleo zitakazokusaidia. 7. Anza kujinunulia assets kama ardhi na nyinginezo. 8. Jifunze kuvaa vizuri na kwa heshima, si tu ilimradi umependeza. 9. Kubali sasa kwamba umekua na acha tabia na mambo ya kitoto. 10. Yaache ya zamani yapite na anza mapya. Mwajuma huna mpango naye, achana naye. Acha kurudi rudi nyuma!

JIFUNZE KALENDA YA UZAZI

Hii ni njia ambayo mwanamke anaweza kutumia kupanga uzazi bila kutumia dawa au kitu cha aina yoyote.  Njia hii inategemea kuchagua kwa makini siku za kufanya mapenzi kutegemeana na ufahamu wa kipindi chote cha hedhi cha mwanamke. Njia hii ina faida yake, lakini yeyote anayeitumia lazima awe makini sana, kwa sababu lazima ajue lini anategemea kupata damu ya hedhi tena.  Ni rahisi sana kufanya makosa kwa kutumia njia hii, kwa hiyo pamoja na kutoa maelezo ya jinsi ya kutumia, sisi hatumshauri mtu kutumia njia hiyo.  Nani anaweza kutumia njia ya kalenda Moja,  Wanawake walioko tayari kuchukua miezi 3 hadi 6 kupima vipindi vyao vya hedhi kabla ya kutumia njia hiyo. Pili,  Wanawake walio na mzunguko wa hedhi ambayo urefu wake haubadiliki. Tatu, Wanawake wanaojua hisabati vizuri sana.  Kwa hiyo, kabla ya kutumia njia hiyo, ni vyema kwa mwanamke kuandaa kalenda inayoonesha siku yake ya kwanza kutoa damu ya hedhi kila mwezi kwa kipindi cha miezi 3 ha...

JE UNAMJUA ALIYETUNGA WIMBO WA TAIFA? HUYU APA

HUYU NDIYE MTUNZI WA WIMBO WA TAIFA WA TANZANIA JE, unamfahamu mtu aliye tunga sauti (melody ) ya wimbo ambao leo Watanzania wanaiita Wimbo wa Taifa? Huyu ni Enock Sontonga , raia wa Afrika Kusini, aliye tunga mashairi ya wimbo wa ‘Mungu Ibariki Afrika’ ambao kwa lugha moja ya Afrika Kusini unajulikana kama ‘Nkosi Sikelel’ i Afrika’. Sontonga alizaliwa mwaka 1873 na kufariki Aprili 18, 1905. Sauti ya wimbo huo u metumiwa na nchi kadhaa kwa nyimbo za taifa za  Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia, Zambia na Tanzania ambapo Tanzania na Zambia zimeendelea kuitumia ‘melody’ hiyo hadi leo hii. Nchi zingine tatu za Wazimbabwe , Nami bia na Afrika Kusini imetungwa nyimbo nyingine. Wimbo huu ulitungwa mwaka 1897  na kurekebishwa na wahariri mbalimbali mpaka kufikia kutumika vyema katika maswala ya kitaifa.