Skip to main content

NAJIVUNIA TANZANIA

ZIJUE HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA NA WAKATI MZURI WA KUTEMBELEA



BAADHI YA HIFADHI ZA TAIFA KATIKA PICHA JINSI ZINAVYOONEKANA

Na, Gordon Kalulunga

WATANZANIA wengi kutokana na mazoea kuwa wanaotakiwa kutembelea hifadhi za Taifa ni watalii wa nje ya nchi, wameshindwa kujitokeza kwa wingi kutembelea hifadhi hizo kutokana na sababu mbalimbali.

Moja ya sababu ya kutoweza kutembelea hifadhi hizo ni pamoja na hofu ya viingilio wakifika katika hifadhi hizo jambo ambalo naamini kuwa baada ya kusoma makala hii wengi wetu tutabadili fikra zetu na kujitokeza katika kutembelea vivutia vya utalii vilivyopo kila pembe ya nchi yetu.

Baadhi ya vivutio ambavyo vinasimamiwa kikamilifu na Shirika la Hifadhi za Taifa la Tanzania (TANAPA) ni pamoja na hifadhi ya Taifa ya Arusha, Gombe, Katavi, Mlima Kilimanjaro, Mahale, Mikumi, Manyara, Ruaha, Rubondo, Serengeti, Saadan, Tarangire, Udzungwa, Kitulo, Mkomazi na Saanane.

Katika Hifadhi hizo za taifa unapotembelea kuna tozo zake ambapo Ada ya kuingilia Hifadhi za Serengeti, Kilimajaro, Arusha, Tarangire, Gombe, Mahale na Manyara mtu mzima kuanzia miaka 16 na kuendelea analipa Sh.1,500, Miaka 5 na 16 Sh. 500 na miaka chini ya 5 ni bure.

Hifadhi za Katavi, Mikumi, Ruaha, Rubondo,Saadani, Kitulo na Udzungwa ada yake kwa mtu wa miaka 16 na kuendelea analipa Sh.1,000, kati ya 5 mpaka 16 analipa Sh.500 na chini ya miaka mitano ni bure, vivyo hivyo ada za kambi za Jumuiya (Public).

Ila katika kambi Maalum (Special) mtu wa miaka 16 na zaidi analipa Sh.2,000, miaka mitano na 16 wanalipa Sh.1,000 na wale wa miaka chini ya mitano ni bure na waongoza wageni wanalipwa Sh.500 na ambao wanataka kutalii mida ya nje ya saa za kazi wanamlipa Sh.1000.

Arusha
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA) Ahmed Mbugi anagusia kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Arusha kuwa ina ukubwa wa kilomita za mraba 328.4, iko umbali wa kilomita 62 (kiasi cha mwendo wa saa moja kwa gari) kutoka mji wa kitalii wa Arusha.

‘’Hifadhi hii ina maeneo matatu muhimu ambayo ni bonde la Ngurdoto (Ngurdoto Crater), maziwa ya Momella ambayo kila moja hutoa mandhari tofauti pamoja na Mlima Meru wenye urefu wa mita 4566 (futi 14990), hali ambayo inaifanya hifadhi kuwa na mazingira ya baridi’’ anasema Mbugi.

Ikumbukwe kuwa hifadhi hii ni maarufu kwa wanyama jamii ya tumbili wajulikanao kama Mbega weusi na weupe. Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hii ni pamoja na Twiga,pundamilia, Nyati na digidigi.

Unaweza kuwaona Chui wakibarizi katika vivuli vya matawi ya miti inayokingwa na maaguko ya maji huku makundi kadhaa ya batamaji yakitafuta wadudu katika maziwa ya Momella.
Zaidi ya aina 400 za ndege wamethibitika kupatikana ndani ya hifadhi hii. Safari za miguu na kupanda milima Meru ni moja ya burudani muhimu katika hifadhi ambapo mpandaji anahitaji kati ya siku 3-4 za kupanda mlima.

Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kati ya mwezi Juni na Februari ingawa mvua inaweza kunyesha mwezi Novemba. Kuna maeneo ya malazi ndani ya hifadhi yenye hadhi tofautitofauti kama hoteli, nyumba za wageni na makambi ya kupuga mahema ingawa wageni pia wanawezakupata malazi eneo nje ya hifadhi katika mji wa Usa River na Arusha mjini.

Gombe
Hifadhi ya Taifa ya Gombe ni ndogo kuliko zote nchini ikiwa na jumla ya kilomota za mraba 52 lakini ina umaarufu mkubwa unaotokana na kuwa na wanyama aina ya Sokwe.

Gombe ni moja ya makzi ya machache yaliyosalia ya Sokwe duniani. Ipo kilomita 16 kaskazini mwa mji wa Kigoma, hifadhi hii ni ukanda mwembamba wa msitu wa mlima unaokatizwa na miteremko mikali inayoingia katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika.

Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hii ni pamoja na Kima wenye mikia myekundu na kima wa rangi ya bluu na wale wanyama jamii ya Paka hawapo katika hifadhi hii kama vile Simba na Chui hivyo kuifanya kuwa salama kwa safari za miguu.

Unaweza kwenda kutembelea hifadhi hii kwa ndege za abiria au za kukodi kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma mjini na baadaye kwa boti mpaka makao makuu ya hifadhi, kadhalika kuna huduma za treni kutoka Mwanza na Dar es Salaam pamoja na barabara itokayo Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam.

Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni wakati wa kiangazi, Julai mpaka Octoba kwani Sokwe hawapendi kutembea nyakati za mvua.

Katavi
Hifadhi ya Taifa ya Katavi, ina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 4471, iko juu ya uwanda mpana wa mafuriko kusini magharibi mwa Tanzania katika mkoa wa Katavi zamani Rukwa. Mandhari kuu katika hifadhi hii ni maeneo yenye maji maji  yene majani, mimea mithili ya mitende pamoja na mto Katuma.

Katavi inasifika kwa kuwa na idadi kubwa ya Mambo na voboko na ni kawaida kuyaona makundi makubwa ya Tembo ya kila majani katika mabwawa huku miili yao ikiwa imefunikwa na maji na magugu.

Hifadhi hii inafikiwa kwa ndege za kukodi kutoka Dar es Salaam na Arusha  na kwa Gari kutoka Mbeya na pia kwa kupitia mkoani Kigoma wakati wa kiangazi Mei-Octoba na kuanzia katikati ya Desemba hadi Februari. Inafikika pia kwa reli kutoka Dar es Salaam kupitia Tabora hadi mpanda na kwa gari kutoka Mpanda.

Mahale.
Hifadhi hi inaundwa inaundwa na vilima vilivyojipanga na kufunikwa na misitu minene ikiwa na jumla ya kilomita za Mraba 1613. Kama ilivyo hifadhi ya jirani ya kaskazini ya Gombe, hifadhi ya milima ya Mahale ni makazi ya jamii adimu zilizobakia za sokwe barani Afrika.

Mabaki ya matunda yaliyoliwa na kinyesi kibichi ni miongoni mwa alama zitakazokuongoza mgeni hadi kuwafikia viumbe hawa katika misitu iliyopo katika mlima huo na hifadhi hii ipo Maharibi mwa Tanzania ikiwa inapakana na Ziwa Tanganyika.

Ukifika hapo utaona na sehemu ya asili ya watu wa kabila la Watongwe walipokuwa wakiaabudia mizimu yao milimani, kisha kurudi ziwani na kujitumbukiza kwenye maji baridi na maangavu.

Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kipindi cha kiangazi, kati ya mwezi Mei na Octoba.

Ziwa manyara.
Hifadhi hii ya Taifa ya Ziwa Manyara ni maarufu kwa Simba wanaopanda miti na lipo ndani ya hifadhi ambayo ina ndege wengi zaidi ya aina 400 wanaovutia wakiwemo ndege aina ya Korongo ambao huonekana kama pazia kubwa jeupe.

Idadi kubwa ya wanafunzi hapa nchi wanatembelea hifadhi hii na kujionea maajabu yaliyopo ambapo ni pamoja na kujionea wanyama kama Simba, Nyati, Tembo, Nyani, Chui, Pundamilia, na wanyama wengine wanaokula majani na wanaona chemichemi za maji moto yanayobubujika kutoka ardhini bila kukauka kwa mamilioni ya miaka.

Hifadhi hii ipo umbali wa kilomita 126 kutoka Arusha mjini, na wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kuanzia mwezi June hadi Desemba.

Ruaha.

Hifadhi ya Ruaha ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania ambapo ina ukubwa wa kilomita za mraba 20,226 na ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Afrika baada ya hifadhi ya Kafue iliyopo nchini Zambia.

Ni maarufu kwa kuwa na wanyama aina ya Kudu wakubwa na wadogo ambao hupatikana kwa wingi ambapo hustawi wa hifadhi hii unategemea mto ruaha ambao aina mbalimbali za Samaki, Mamba na viboko hupatikana katika mto huu.

Wanyama kama Pofu na swala hunywa maji katika mto huo wa Ruaha ambao ni mawindo makubwa ya wanyama wakali wakiwemo Simba, Chui, Mbweha, Fisi na Mbwa mwitu. Pia eneo hili Tembo hukusanyika kwa wingi kuliko eneo lolote la hifadhi zilizopo katika nchi za Afrika Mashariki.

Katika hifadhi hii utajionea Magofu yanayosadikiwa kuwa yalikuwa makazi ya watu wa kale katika Kijiji cha Isimila kiasi cha Kilomita 120 kutoka Iringa. Magofu haya ni miongoni mwa historia ya kale barani Afrika.

Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ili kuangaliwa wanyama wakubwa ni wakati wa kiangazi kuanzia Mei hadi Desemba, lakini kuangalia ndege na maua wakati wa masika ni Januari –April .

Rubondo.

Hifadhi hii ya Taifa ni kisiwa ambacho kipo pembezoni mwa Ziwa Victoria, ziwa ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani likiwa linazungukwa na nchi Tatu, Tanzania, Uganda na Kenya.

Kisiwa hiki kinaundwa na visiwa tisa vidogo vidogo ambapo kisiwa hiki cha Rubondo ni makazi na mazingira muafaka ya kuzaliana Samaki wakiwemo Sato na Sangara wenye ukubwa wa uzito wa kilo hadi 100.

Wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni pamoja na Viboko,Pongo, Nzohe, Fisi maji, Mamba na Pimbi, wanabadilishana makazi na wanyama wengine waliohamishiwa katika hifadhi hii kama Sokwe, Tembo, Mbega weusi na weupe na Twiga.

Wakati mzuri wa kutembelea ni wa Kiangazi June-Agosti aidha wakati wa masika Novemba-Machi kwa ajili ya kuona maua na vipepeo na vile vile Desemba-Februari kwa kuwaona ndege wahamiaji.

Saadani.
Hifadhi hii ipo ufukweni mwa bahari ya Hindi na ni hifadhi pekee Afrika Mashariki inayoungana na Bahari na ipo umbali wa Kilomita 100 kaskazini Magharibi mwa Dar es Salaam na umbali kama huo kusini Magharibi mwa bandari ya Tanga.

Ilianzishwa kama pori la akiba mwaka 1960 na ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka 2005 na ukifika hapo unaweza kuona wanyama kama Simba, Chui, Fisi, Tumbili, swala na ngedele na mtalii mbali ya kuona wanyama pia unapata nafasi ya kuogelea na wakati wa kutembelea ni wakati wowote kwa mwaka ingawa wakati wa masika barabara zinaweza kutopitika kirahisi.

Udzungwa.
Hifadhi hii ya Milima ya Udzungwa ina hazina nyingi za mimea, ndege na wanyama ambao hazipatikani sehemu nyingine duniani.

Kati ya aina sita za jamii ya nyani wanapatikana katika hifadhi hii, mbili hupatikana katika hifadhi hii pekee; Mbega mwekundu wa Iringa (Iringa red colobus Monkey) na Sanje Crested mangabey’’ ambaye alikuwa hajulikani hadi mwaka 1979 na ndege mbalimbali.

Kivutio kikubwa zaidi ni Mto Sanje ambao unatoa maporomoko ya maji yenye urefu wa mita zipatazo 170 yakianguka kupitia msituni na kutua mithili ya mianzo ya ukungu bondeni.

Kitulo.
Awali hifadhi hii ilijulikana kwa jina la Elton Plateau baada ya Mvumbuzi Fredrick Elton kupia eneo hili mnamo mwaka 1870, mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO)ilichukua eneo hili kwa ajili ya ukulima wa ngano na ufugaji wa Kondoo.

Baadaye likageuzwa kuwa shamba la Ng’ombe ambalo lipo hadi leo. Mwaka 2005 Kitulo likatangazwa kuwa hifadhi ya Taifa na ni hifadhi ambayo ina maua aina mbalimbali na zaidi ya aina 30 hupatikana Kitulo pekee.

Pia ndiyo eneo pekee Tanzania ambapo ndege aina ya Tandawala  machaka (Denhams Bustard) wana makazi na ndani ya hifadhi hii kuna miti aina ya Cidar yenye urefu wa zaidi ya mita 50 na inakadiliwa kuwa mirefu kuliko yote duniani.

Kitulo inafikiwa kwa gari kutoka Chimala kilomita 78 Mashariki mwa mji wa Mbeya. Reli ya TAZARA hupita karibu na hifadhi hii.

Kupitia makala haya ni muhimu wananchi kila mmoja wetu kupata mwamuko wa kutembelea Hifadhi zetu kwa ajili ya kujifunza historia na kujua mambo mbalimbali na kupana ufahamu mkubwa wa uhifadhi na utunzaji wa Mazingira.

Makala hii pia itachapwa katika Gazeti la Tanzania Daima hivi karibuni.

Comments

Popular posts from this blog

MAMBO KUMI YA KUFANYA KABLA YA MIAKA 25

1. Jifunze kuweka akiba ya fedha na iache bila kuigusagusa.   2. Tafuta mpenzi sahihi na tulia naye, panga maisha. 3. Ishi mahali pa peke yako, acha kuishi kwa wazazi au kupanga na nyumba na washkaji. 4. Lipa madeni yako ya zamani. Yote! 5. Tengeneza mwili ambao unataka halafu jitahidi kuu-maintain! Anza kuzingatia kuishi kwa kujali afya yako sana. 6. Jitahidi uwe na marafiki ambao wana changamoto za kimaendeleo zitakazokusaidia. 7. Anza kujinunulia assets kama ardhi na nyinginezo. 8. Jifunze kuvaa vizuri na kwa heshima, si tu ilimradi umependeza. 9. Kubali sasa kwamba umekua na acha tabia na mambo ya kitoto. 10. Yaache ya zamani yapite na anza mapya. Mwajuma huna mpango naye, achana naye. Acha kurudi rudi nyuma!

JIFUNZE KALENDA YA UZAZI

Hii ni njia ambayo mwanamke anaweza kutumia kupanga uzazi bila kutumia dawa au kitu cha aina yoyote.  Njia hii inategemea kuchagua kwa makini siku za kufanya mapenzi kutegemeana na ufahamu wa kipindi chote cha hedhi cha mwanamke. Njia hii ina faida yake, lakini yeyote anayeitumia lazima awe makini sana, kwa sababu lazima ajue lini anategemea kupata damu ya hedhi tena.  Ni rahisi sana kufanya makosa kwa kutumia njia hii, kwa hiyo pamoja na kutoa maelezo ya jinsi ya kutumia, sisi hatumshauri mtu kutumia njia hiyo.  Nani anaweza kutumia njia ya kalenda Moja,  Wanawake walioko tayari kuchukua miezi 3 hadi 6 kupima vipindi vyao vya hedhi kabla ya kutumia njia hiyo. Pili,  Wanawake walio na mzunguko wa hedhi ambayo urefu wake haubadiliki. Tatu, Wanawake wanaojua hisabati vizuri sana.  Kwa hiyo, kabla ya kutumia njia hiyo, ni vyema kwa mwanamke kuandaa kalenda inayoonesha siku yake ya kwanza kutoa damu ya hedhi kila mwezi kwa kipindi cha miezi 3 ha...

JE UNAMJUA ALIYETUNGA WIMBO WA TAIFA? HUYU APA

HUYU NDIYE MTUNZI WA WIMBO WA TAIFA WA TANZANIA JE, unamfahamu mtu aliye tunga sauti (melody ) ya wimbo ambao leo Watanzania wanaiita Wimbo wa Taifa? Huyu ni Enock Sontonga , raia wa Afrika Kusini, aliye tunga mashairi ya wimbo wa ‘Mungu Ibariki Afrika’ ambao kwa lugha moja ya Afrika Kusini unajulikana kama ‘Nkosi Sikelel’ i Afrika’. Sontonga alizaliwa mwaka 1873 na kufariki Aprili 18, 1905. Sauti ya wimbo huo u metumiwa na nchi kadhaa kwa nyimbo za taifa za  Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia, Zambia na Tanzania ambapo Tanzania na Zambia zimeendelea kuitumia ‘melody’ hiyo hadi leo hii. Nchi zingine tatu za Wazimbabwe , Nami bia na Afrika Kusini imetungwa nyimbo nyingine. Wimbo huu ulitungwa mwaka 1897  na kurekebishwa na wahariri mbalimbali mpaka kufikia kutumika vyema katika maswala ya kitaifa.