WABUNGE wameibana serikali ieleze maandalizi yake kwenye ulinzi wa hifadhi ya madini itakayokuwa kwenye Benki Kuu (BoT) kabla ya kuyauza.
Hatua hiyo ilitokana na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi kuwasilisha maelezo ya serikali kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2017, kwa Kamati ya Katiba na Sheria juzi mjini hapa.
Miongoni mwa wabunge waliohoji ni pamoja na Mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Rashid Akibar akibainisha kuwa hapo awali BoT iliwahi kutunza dhahabu na baada ya muda vikautwaa mchanga na si dhahabu tena. Alitaka waziri Kabudi atoa ufafanuzi wa jambo hilo.
“Serikali iko tayari kuchukua ulinzi nchini Marekani?” Alihoji mbunge huyo.
Naye Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), John Heche alisema jengo la BoT liliwahi kuungua na kuuliza Serikali inalichukulije jambo hilo "ili Watanzania wasijeingia katika matatizo.”
Kwa pande wake, Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Almasi Maige alibainisha utaalamu wa BoT ni utunzaji wa fedha na si dhahabu, hivyo kuitaka Serikali ijiridhishe katika jukumu hilo jipya kwa Benki Kuu.
Kadhalika, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma aliishauri Serikali kabla ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo ni vyema ikaiongezea ulinzi BOT.
Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu alitaka kujua kama serikali imeangalia uzoefu kutoka nchi nyingine kabla ya kuandika muswada huo.
Akijibu hoja za wabunge, Prof. Kabudi aliwataka wabunge kutokuwa na hofu kuhusu usalama wa BoT kwa sababu wakati jengo linaungua lilikuwa na mbao nyingi.
Alisema teknolojia imekuwa kwa kuwekwa vifaa vya utambuzi wa moto.
Kuhusu uzoefu, Waziri Kabudi alisema wameangalia uzoefu katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Botswana, Sierra Leone, Indonesina, Saud Arabia na Ghana.
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment