Skip to main content

JUA UGOJWA HATARI WA HIMOFILIA

TAKRIBANI Watanzania 5,400 wanaugua ugonjwa wa himofilia, huku wataalamu wakibainisha kuwa wanaojulikana na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ni 100 pekee.
Himofilia ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda pale mtu anapopata jeraha, kwa kukosa kiwango cha kutosha cha chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu na kusababisha damu kuvuja kwa muda mrefu.

Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Damu wa MNH, Dk. Stella Rwezaura, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo uliogundulika mwaka 2009.

Alisema takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania 10,000, mmoja anaugua ugonjwa huo ambao kwa asilimia 70 unatokana na kurithi kutoka kwenye vinasaba vya kike na asilimia 30 kwa mabadiliko ya vinasaba.

“Watanzania wengi hupeleka watoto wao kwenda jando bila kuwapima kama wana ugonjwa wa himofilia au la, na wapo wanaopoteza maisha kwa sababu hiyo, ni muhimu kuwapima hata kabla ya upasuaji,” alisema.

Alisema kwa sasa kuna madaktari bigwa wa damu 10 pekee nchini huku wahudumu wa afya wengi wakiwa hawana uelewa wa ugonjwa huo tishio.

Kwa mujibu wa Rwezaura tiba ya ugonjwa huo huanza kutolewa tangu mtoto anapokuwa na umri wa miaka mitatu na hufundishwa kujichoma sindano maalumu za dawa hizo anapofikisha umri wa miaka nane. Dk.

Rwezaura alisema kuna aina tatu za himofilia ambazo ni pamoja na himofilia A inayowapata wengi kwa kukosa chembechembe za kugandisha damu.

Nyingine ni himofilia B ambayo huwapata wagonjwa wachache wenye upungufu wa chembechembe namba tisa na wenye himofilia A na B ambayo mgonjwa huvuja damu kwa muda mrefu kuliko kawaida.

Alibainisha kuwa mgonjwa anaweza kupoteza maisha kwa kuvuja damu nyingi bila matibabu kwa kuwa hakuna chembechembe za kuzuia damu kutoka na kwamba viunganishi vya mwili, mfano magoti, kiwiko na uti wa mgongo wakati mwingine huvimba kutokana na damu kuvujia ndani na baadaye kusababisha ulemavu. Dk. Rwezaura alisema himofilia mbaya zaidi ni ile ambayo damu huvujia kwenye ubongo kwa kuwa ni nadra mgonjwa kupona.

"Hadi sasa, hospitali inayotibu ugonjwa huo ni Muhimbili tu. KCMC na Bugando wanatoa vipimo vya awali," alisema.

Awali akisoma hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, juu ya ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza, Prof. Ayoub Magimba, alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2008, zinaonyesha kuwa takribani vifo milioni 36 duniani vilitokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ukiwamo ugonjwa huo.

“Kulingana na takwimu za Shirika la Himofilia Duniani (WHF), watu 400,000 wanaishi na himofilia duniani. Kati yao, asilimia 25 ndiyo wanaopata matibabu,” alifafanua Prof. Magimba.

Katika hotuba hiyo, Waziri Ummy alisema serikali inatambua kuwa ugonjwa huo ni mkongwe kama maeneo mengine duniani, lakini jamii haina ufahamu wa kutosha na kwamba wengi wa wataalamu wa tiba nao hawana ufahamu wa kutosha pia.

Waziri huyo alisema inakadiriwa kuwa asilimia 97 ya watu wenye himofilia hawajui kama wanao na hawajawahi kupima na kwamba utafiti umebainisha kuwa hatua madhubuti zikichukuliwa, mgonjwa ataweza kuishi maisha ya kawaida bila kuathiri mwili na kuepuka kupata ulemavu.

Alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili jamii ya watu wenye himofilia ni uelewa mdogo, dawa na vipimo tiba, wataalamu wa tiba kutokuwa na uelewa wa kutosha, waganga wa tiba asili na ghariba kufanya tohara bila tahadhari.

Waziri huyo alizitaja changamoto nyingine kuwa ni wazazi na wagonjwa kukosa uelewa na ukosefu wa vituo maalumu vya kuhudumia wagonjwa zaidi ya Muhimbili.

“Tanzania imedhamiria kushirikiana na wadau wa himofilia katika kufikisha elimu ya uenezi katika jamii nzima. Serikali itaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ambayo iko kwenye hatua za mwisho za marekebisho,” alifafanua zaidi Ummy katika hotuba hiyo.

Rais wa Chama cha Himofilia Tanzania, Richard Minja alisema madhara yaliyojitokeza katika familia ni wanaume kuzikimbia familia zao baada ya watoto kubainika kuwa na ugonjwa huo.

Alisema ni lazima kuwe na utekelezaji wa kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni 'uvujaji damu, ulemavu na vifo vitokanavyo na himofilia sasa basi'.

Minja alisema kwa sasa dawa za ugonjwa huo zinatolewa kwa msaada na watu wa Marekani na kwamba mgonjwa kupata dawa za mwaka mzima anatakiwa kuwa na dola za Marekani 100,000 (zaidi ya Sh. milioni 200), lakini kwa sasa matibabu yanatolewa bure nchini.

“Mgonjwa anatakiwa kuongezewa chembechembe mara mbili kwa wiki, pia inashauriwa awe nazo muda wote nyumbani ili inapotokea ameumia anatumia. Pia wanatakiwa kufanya mazoezi na kuepuka kuumia,” alisema.

Aliitaja tiba nyingine ya ugonjwa huo kuwa ni 'plasma' inayotokana na chembechembe za damu ya watu wengine ambapo wataalamu huchuja chembechembe hizo kutoka kwenye benki za damu.

Alisema katika kliniki ya Muhimbili kuna wastani wa wagonjwa watano hadi 10 kwa wiki wanaoendelea na matibabu. “Damu ikivuja kwa muda mrefu bila matibabu husababisha madhara makubwa na hata kifo, kwani huathiri magoti, mifupa ya fahamu na kusababisha ulemavu.

Kifo hutokea iwapo damu itavuja kwa muda mrefu kwenye viungo muhimu kama ubongo, uti wa mgongo na tumbo bila kutibiwa," alisema.

Minja alisema kuna dawa maalumu za sindano za ugonjwa huo na wagonjwa hawapaswi kumeza dawa za kutuliza maumivu isipokuwa panadol.

Abdulsaid Mgima, mgonjwa wa himofilia, alisema aligundulika kuwa na ugonjwa huo akiwa na umri wa miaka 10 akiwa mkoani Mbeya baada ya wazazi wake kuhangaika kumtibu bila mafanikio hadi alipopelekwa Muhimbili. "Ugonjwa ulianzia kwenye mkono (umepinda), lakini naendelea na shughuli zangu.

Ninaiomba serikali itambue ugonjwa huu na kuwafikia watu wengi zaidi hususani vijijini," alisema. Cecilia Swai alisema kuwa alipoteza mtoto mwaka 2013 kutokana na ugonjwa huo baada ya kukosa dawa za ugonjwa huo.

Alisema mtoto wake aliugua kwa siku tatu na alipofikishwa Muhimbili, hakukuwa na dawa za kumsaidia hivyo akafariki dunia. Kwa mujibu wa Dk. Rwezaura, wagonjwa sita walipoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu Muhimbili kabla hospitali hiyo haijapata dawa ya kutibu ugonjwa huo.

Comments

Popular posts from this blog

Aina bora za ng’ombe wa maziwa, banda na namna ya kuanza ufugaji

Uzalishaji wa maziwa ni biashara nzuri sana na ya kuvutia ambayo huwa na faida nyingi na humfanya mfugaji kuridhika hasa kwa yule anayependa kazi hii. Hata hivyo, ni lazima kuanza kwa kuweka msingi imara hata kabla ya kufikiria ni aina gani ya mbegu utaichukua kwa ajili ya kufuga. Ni vizuri kufahamu kuwa, usimamizi ni moja ya jambo muhimu sana ambalo likifanyiwa uzembe linaweza hata kumbadilisha ng’ombe wa maziwa kuwa na uzalishaji duni kama ngo’mbe wa kienyeji. Aina mbalimbali za ng’ombe wa maziwa huwa na mahitaji tofauti, hivyo kiwango cha maandalizi yako ni muhimu sana. Unahitajika kufahamu kuwa, unalazimika kufikia mahitaji yako kwa ajili ya lishe, si kwenye mahitaji ya awali tu bali pamoja na mahitaji ya baadaye ya ngo’mbe wako. Suala hili limefanya wafugaji wengi kushindwa kuendelea kutokana na kuwa hujiingiza katika shughuli hii bila kuangalia mambo ya msingi yanayotakiwa pamoja na kuweka mipango thabiti. Pamoja na kuwa mahitaji yote kwa ajili ya lishe na mambo me...

NAJIVUNIA TANZANIA

ZIJUE HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA NA WAKATI MZURI WA KUTEMBELEA   BAADHI YA HIFADHI ZA TAIFA KATIKA PICHA JINSI ZINAVYOONEKANA Na, Gordon Kalulunga WATANZANIA wengi kutokana na mazoea kuwa wanaotakiwa kutembelea hifadhi za Taifa ni watalii wa nje ya nchi, wameshindwa kujitokeza kwa wingi kutembelea hifadhi hizo kutokana na sababu mbalimbali. Moja ya sababu ya kutoweza kutembelea hifadhi hizo ni pamoja na hofu ya viingilio wakifika katika hifadhi hizo jambo ambalo naamini kuwa baada ya kusoma makala hii wengi wetu tutabadili fikra zetu na kujitokeza katika kutembelea vivutia vya utalii vilivyopo kila pembe ya nchi yetu. Baadhi ya vivutio ambavyo vinasimamiwa kikamilifu na Shirika la Hifadhi za Taifa la Tanzania (TANAPA) ni pamoja na hifadhi ya Taifa ya Arusha, Gombe, Katavi, Mlima Kilimanjaro, Mahale, Mikumi, Manyara, Ruaha, Rubondo, Serengeti, Saadan, Tarangire, Udzungwa, Kitulo, Mkomazi na Saanane. Katika Hifadhi hizo za taifa unapotembelea kuna tozo zak...

Mawazo Yakinifu Ya Mafanikio Endelevu Kwako

Mafanikio yoyote yanaanza na mawazo. Hakuna mafanikio yanazaliwa nje ya mawazo. Kwa jinsi unavyokuwa na mawazo bora ndivyo unavyozidi kuwa na mafanikio bora kwako. Mawazo bora unayapata vipi, unayapata kwa kujifunza. Kupitia makala haya, nakukaribisha tujifunze pamoja mawazo yakinifu ya mafanikio yako endelevu. Naamini kupitia mawazo haya, utajifunza kitu ambacho kitakutoa hatua moja na kwenda hatua nyingine, karibu tujifunze. 1.Unaweza ukaendelea kuteseka kila siku na maisha na kuteseka kila na kila aina ya ugonjwa, lakini hiyo yote inaweza ikasababishwa na ujinga ambao  umeushikilia. Ujinga ni adui mkubwa sana wa mafanikio yako. Fanya ufanyalo, futilia mbali ujinga wote ambao upo kwako. Ukifuta ujinga utakuweka huru na utaishi maisha ya mafanikio. Wajinga ndio waliwao na ujinga haumfanikishi mtu, tadhari usiwe kichaka cha ujinga, UTAKWAMA. 2. Kwa mawazo uliyonayo ujue kabisa yanatengeza dunia yako, yanatengeneza maisha yako au yanaumba maisha yako. Swala la kuwa makini sana kw...